요한복음 15장 Swahili
Swahili · 스와힐리어 · 요한복음 (John) · 27절
- 1 "Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.
- 2 Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi.
- 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni.
- 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu.
- 5 "Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote.
- 6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue.
- 7 Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa.
- 8 Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu.
- 9 Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu.
- 10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
- 11 Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike.
- 12 Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.
- 13 Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
- 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.
- 15 Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu.
- 16 Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho kwa jina langu.
- 17 Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni.
- 18 "Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi.
- 19 Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni.
- 20 Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia.
- 21 Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma.
- 22 Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi.
- 23 Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia.
- 24 Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia.
- 25 Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: Wamenichukia bure!
- 26 "Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.
- 27 Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo.
Swahili — getbible.net(CrossWire SWORD 모듈)에서 가져옴 · 라이선스: 공개 도메인 (Public Domain)