요한복음 16장 Swahili
Swahili · 스와힐리어 · 요한복음 (John) · 33절
- 1 "Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu.
- 2 Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu.
- 3 Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi.
- 4 Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni. "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
- 5 Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: Unakwenda wapi?
- 6 Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu.
- 7 Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu.
- 8 Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.
- 9 Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini;
- 10 kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena;
- 11 kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.
- 12 "Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili.
- 13 Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia, na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja.
- 14 Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
- 15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
- 16 "Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!"
- 17 Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia: Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona? Tena anasema: Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!"
- 18 Basi, wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: Bado kitambo kidogo? Hatuelewi anaongelea nini."
- 19 Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?
- 20 Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi: mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
- 21 Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani.
- 22 Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.
- 23 Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni.
- 24 Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike.
- 25 "Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba.
- 26 Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu;
- 27 maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.
- 28 Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba."
- 29 Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo.
- 30 Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu."
- 31 Yesu akawajibu, "Je, mnaamini sasa?
- 32 Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami.
- 33 Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!"
Swahili — getbible.net(CrossWire SWORD 모듈)에서 가져옴 · 라이선스: 공개 도메인 (Public Domain)