요한복음 14장 Swahili
Swahili · 스와힐리어 · 요한복음 (John) · 31절
- 1 Yesu aliwaambia, "Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia.
- 2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; la sivyo ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.
- 3 Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.
- 4 Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda."
- 5 Thoma akamwuliza, "Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?"
- 6 Yesu akamjibu, "Mimi ni njia, na ukweli na uzima. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.
- 7 Ikiwa mnanijua mimi mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona."
- 8 Filipo akamwambia, "Bwana, tuonyeshe Baba, nasi tutatosheka."
- 9 Yesu akamwambia, "Filipo, nimekaa nanyi muda wote huu, nawe hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: Tuonyeshe Baba?
- 10 Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni nyote siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake.
- 11 Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.
- 12 Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, maana nakwenda kwa Baba.
- 13 Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
- 14 Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.
- 15 "Mkinipenda mtazishika amri zangu.
- 16 Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele.
- 17 Yeye ni Roho wa kweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.
- 18 "Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja tena kwenu.
- 19 Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.
- 20 Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu.
- 21 Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."
- 22 Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, "Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?"
- 23 Yesu akamjibu, "Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye.
- 24 Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
- 25 "Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi
- 26 lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.
- 27 "Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi ninyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
- 28 Mlikwisha sikia nikiwaambieni: Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu. Kama mngalinipenda mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi.
- 29 Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini.
- 30 Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;
- 31 lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!"
Swahili — getbible.net(CrossWire SWORD 모듈)에서 가져옴 · 라이선스: 공개 도메인 (Public Domain)