요한복음 13장 Swahili
Swahili · 스와힐리어 · 요한복음 (John) · 38절
- 1 Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho!
- 2 Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu.
- 3 Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu.
- 4 Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni.
- 5 Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia.
- 6 Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, "Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?"
- 7 Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye."
- 8 Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena."
- 9 Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia."
- 10 Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Ninyi mmetakata, lakini si nyote."
- 11 (Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: "Ninyi mmetakata, lakini si nyote.")
- 12 Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?
- 13 Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi.
- 14 Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu.
- 15 Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni.
- 16 Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma.
- 17 Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
- 18 "Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.
- 19 Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa mimi ndimi.
- 20 Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma."
- 21 Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!"
- 22 Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani.
- 23 Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.
- 24 Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: "Mwulize anasema juu ya nani."
- 25 Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, "Bwana, ni nani?"
- 26 Yesu akajibu, "Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye." Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.
- 27 Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, "Unachotaka kufanya, kifanye haraka!"
- 28 Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.
- 29 Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa fedha, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini.
- 30 Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.
- 31 Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, "Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
- 32 Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara.
- 33 "Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu. Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: Niendako ninyi hamwezi kwenda!
- 34 Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.
- 35 Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu."
- 36 Simoni Petro akamwuliza, "Bwana, unakwenda wapi?" Yesu akajibu, "Niendako huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye."
- 37 Petro akamwambia "Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Niko tayari kufa kwa ajili yako!"
- 38 Yesu akajibu, "Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili yangu? Kweli nakwambia, kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!"
Swahili — getbible.net(CrossWire SWORD 모듈)에서 가져옴 · 라이선스: 공개 도메인 (Public Domain)