요한복음 2장 Swahili
Swahili · 스와힐리어 · 요한복음 (John) · 25절
- 1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo,
- 2 naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
- 3 Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!"
- 4 Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado."
- 5 Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni."
- 6 Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha.
- 7 Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu.
- 8 Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu."
- 9 Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi,
- 10 akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!"
- 11 Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
- 12 Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.
- 13 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu.
- 14 Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng'ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.
- 15 Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao.
- 16 Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
- 17 Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba yako waniua."
- 18 Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?"
- 19 Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu."
- 20 Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?"
- 21 Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake.
- 22 Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema Yesu.
- 23 Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya.
- 24 Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.
- 25 Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.
Swahili — getbible.net(CrossWire SWORD 모듈)에서 가져옴 · 라이선스: 공개 도메인 (Public Domain)