요한복음 1장 Swahili
Swahili · 스와힐리어 · 요한복음 (John) · 51절
- 1 Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
- 2 Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
- 3 Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
- 4 Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
- 5 Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
- 6 Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,
- 7 ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini.
- 8 Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
- 9 Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
- 10 Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua.
- 11 Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
- 12 Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.
- 13 Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
- 14 Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
- 15 Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa."
- 16 Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
- 17 Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo.
- 18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
- 19 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?"
- 20 Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi siye Kristo."
- 21 Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, "La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu, "La!"
- 22 Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma."
- 23 Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana."
- 24 Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
- 25 Basi, wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?"
- 26 Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
- 27 Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake."
- 28 Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
- 29 Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
- 30 Huyu ndiye niliyesema juu yake: Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!
- 31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua."
- 32 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
- 33 Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.
- 34 Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu."
- 35 Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
- 36 Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu."
- 37 Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
- 38 Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?"
- 39 Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
- 40 Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
- 41 Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" (maana yake Kristo).
- 42 Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, "Mwamba.")
- 43 Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, "Nifuate."
- 44 Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
- 45 Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti."
- 46 Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone."
- 47 Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake."
- 48 Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona."
- 49 Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!"
- 50 Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya."
- 51 Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu."
Swahili — getbible.net(CrossWire SWORD 모듈)에서 가져옴 · 라이선스: 공개 도메인 (Public Domain)